"Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi." (Ufunuo 3:21)
Yesu anamaanisha nini anaposema hivi kwa kanisa la Laodikia? Kuketi na Yesu kwenye kiti chake cha enzi? Kweli?
Hii ni ahadi kwa kila mtu ashindaye, yaani, anayesonga mbele kwa imani hadi mwisho (1 Yohana 5:4), licha ya kila maumivu ya kutisha, na mvuto na furaha ya dhambi. Kwa hiyo ikiwa wewe ni muumini wa kweli wa Yesu, utakaa kwenye kiti cha enzi cha Mwana wa Mungu aketiye kwenye kiti cha enzi cha Mungu Baba.
Ninachukua “kiti cha enzi cha Mungu” kuashiria haki na mamlaka ya kutawala ulimwengu. Hapo ndipo Yesu ameketi. “Lazima atawale,” Paulo alisema, “mpaka awaweke adui zake wote chini ya miguu yake” (1 Wakorintho 15:25). Kwa hiyo, Yesu anaposema, “nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi,” anatuahidi kwamba tutashiriki katika utawala wa vitu yote.
Yesu anajaza ulimwengu kwa utawala wake tukufu kupitia sisi.
Je, hiki ndicho anachofikiria Paulo katika Waefeso 1:22–23? “Akavitia vitu vyote chini ya miguu yake [Kristo] akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa, ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayevijaza vyote katika yote.”
Sisi, kanisa, ndio “ukamilifu wake yeye anayevijaza vyote.” Hii ina maana gani? Ninaichukua hii kumaanisha kwamba ulimwengu utajazwa na utukufu wa Bwana (Hesabu 14:21). Na mwelekeo mmoja wa utukufu huo utakuwa upanuzi kamili na usio na kipingamizi wa utawala wake kila mahali.
Kwa hiyo, andiko la Waefeso 1:23 lingemaanisha: Yesu anajaza ulimwengu kwa utawala wake tukufu kupitia sisi. Kushiriki katika utawala wake, sisi ni utimilifu wa utawala wake. Tunatawala kwa niaba yake, kwa uwezo wake, chini ya mamlaka yake. Kwa maana hiyo, tunaketi pamoja naye kwenye kiti chake cha enzi.
Hakuna hata mmoja wetu anayehisi hivi kama inavyopaswa. Ni ya kupita kiasi — nzuri sana, ya kushangaza sana. Ndiyo maana Paulo anaomba msaada wa Mungu kwamba “macho ya mioyo yenu [yatiwe nuru], mjue tumaini ambalo aliwaitia ni nini” (Waefeso 1:18).
Bila msaada wa nguvu zote sasa, hatuwezi kuhisi ajabu ya kile ambacho tumekusudiwa kuwa. Lakini ikiwa tutapewa kuhisi hivyo, kama ilivyo kweli, miitikio yetu yote ya kihisia kwa ulimwengu huu itabadilika. Amri za ajabu na kali za Agano Jipya hazitakuwa ngeni kama zilivyoonekana hapo awali.