Makala imeandikwa na John Piper
Mwanzilishi na Mwalimu, desiringGod.org
Maneno yalichongwa kwenye gome la kila mti katika bustani ya Mungu ni, “Lakini Ikifa, huzaa matunda mengi” ( Yohana 12:24 ). Maneno matatu yanatiwa alama katika mwili wa kila Mkristo: “Wewe . . . ume . . . kufa” (Wakolosai 3:3). Na ungamo la dhati la kila mwamini ni, "Nimesulubiwa pamoja na Kristo" (Wagalatia 2:20).
Lakini hii ina maana gani? Nani alikufa nilipo okoka kuwa Mkristo? Jibu: "mwili" wangu ulikufa. "Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili " ( Wagalatia 5:24 ). Lakini "mwili" inamaanisha nini? Sio ngozi yangu. Sio mwili wangu- yaani misuli, mifupa, na viungo vyangu. Ambao unaweza kuwa chombo cha haki (Warumi 6:13). Hapana, sio mwili.
Ni nini sasa? Tunaliona jibu katika aina za kazi ambazo mwili hufanya. “Matendo ya mwili” ni vitu kama vile kuabudu sanamu na ugomvi, hasira na husuda ( Wagalatia 5:19–21 ). Hii ni mitazamo , sio tu matendo machafu ya mwili.
Mwili Ni Nini?
“Gharama katika kuua dhambi ni kubwa sana. Hatuchezi michezo ya vita. Matokeo yake ni mbingU au kuzimu.”
Jambo la karibu zaidi kuwa ufafanuzi wa kibiblia wa mwili ni Warumi 8:7–8 : “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.” Mwili ni yule mimi wa zamani niliyekuwa nikimuasi Mungu. Katika mwili, nilikuwa adui na mkaidi asiyetii. Nililichukia wazo la kukiri kwamba nilikuwa na ugonjwa wa dhambi. Nilikaidi wazo kwamba hitaji langu kubwa kabisa lilikuwa ni Tabibu Mwema wa kuniponya. Katika mwili, niliiamini hekima yangu , si ya Mungu. Kwa hiyo, hakuna kitu nilichofanya katika mwili ambacho kingeweza kumpendeza Mungu, kwa sababu “pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu” ( Waebrania 11:6 ). Mwili haufanyi chochote kutokana na imani.
Kwa hivyo, "mwili" ni yule mimi wa zamani anayejitegemea, asiye na imani. Hiki ndicho kilichokufa Mungu aliponiokoa. Mungu aliibana mishipa kwenye moyo wangu wa jiwe wa zamani usioamini. Na ulipokufa, aliutoa na kunipa moyo mpya ( Ezekieli 36:26 ).
Kuna tofauti gani kati ya moyo huu mpya unaoishi na ule wa zamani uliokufa? Jibu limetolewa katika Wagalatia 2:20 : “Nimesulubiwa pamoja na Kristo. . . . Na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.” Moyo wa zamani uliokufa ulijiamini wenyewe; moyo mpya unamtegemea Kristo kila siku.
Pigana na Dhambi kwa Kumtumaini Yesu
Je, watu waliokufa wanapiganaje na dhambi? Wanapigana na dhambi kwa kumwamini Mwana wa Mungu. Wamekufa kwa uongo wa Shetani. Uongo kama huu: Utakuwa na furaha zaidi ukiyaamini mawazo yako kuhusu jinsi ya kuwa na furaha badala ya kuamini shauri na ahadi za Kristo. Wakristo wamekufa kwa udanganyifu huo. Namna wanavyopigana na Shetani ni kwa kuamini kwamba njia na ahadi za Kristo ni bora kuliko za Shetani.
Njia hii ya kufanya vita na dhambi inaitwa "vita vya imani " ( 1 Timotheo 6:12 ; 2 Timotheo 4:7 ). Ushindi wa vita hivi unaitwa “matendo ya imani ” (1 Wathesalonike 1:3 ; 2 Wathesalonike 1:11). Katika vita hivi, Wakristo "wanakuwa watakatifu kwa imani " ( Matendo 26:18).
“Nguvu ya majaribu yote ni matarajio kwamba yatakufanya uwe na furaha zaidi. Lakini dhambi haitokufanya uwe na furaha zaidi.”
Hebu tufikirie basi kuhusu vita hivi vya imani. Sio kama michezo ya vita kwa kutumia risasi za mpira. Umilele uko hatarini. Warumi 8:13 ni mstari mkuu: “Kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini kama mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. ” Hili limeandikwa kwa wanaokiri kuwa Wakristo, na hoja ni kwamba uzima wetu wa milele unategemeana na vita vyetu dhidi ya dhambi. Haimaanishi kwamba tunapata uzima wa milele kwa kuua dhambi. Hapana, tunapigana "kwa Roho". Mungu atapata utukufu, sio sisi.
Wala Waroma 8:13 haimaanishi kwamba tupigane tukiwa na wasiwasi wa kutokuwa na hakika kuhusu kushinda. Kinyume chake, hata tunapopigana, tuna uhakika kwamba “yeye aliyeanza kazi njema ndani [yetu] ataimaliza hata siku ya Yesu Kristo” ( Wafilipi 1:6 ). Wala Warumi 8:13 haimaanishi kwamba ni lazima tuwe wakamilifu sasa katika ushindi wetu dhidi ya dhambi. Paulo anakataa madai yoyote ya ukamilifu: "Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu. " (Wafilipi 3:12).
Pambano analolitaka Mungu
Hitaji katika Warumi 8:13 si kutokuwa na dhambi, bali ni mapambano ya kufa dhidi ya dhambi. Hii ni muhimu sana katika maisha ya Kikristo. Vinginevyo, hatutoi ushahidi kwamba mwili umesulubiwa. Na ikiwa mwili haukusulubiwa, basi sisi si wa Kristo ( Wagalatia 5:24 ). Gharama katika vita hivi iko juu sana. Hatuchezi michezo ya vita. Matokeo yake ni mbinguni au kuzimu.
Ni jinsi gani basi watu waliokufa “wanafisha matendo (ya dhambi) ya mwili”? Tumejibu, "Kwa imani!" Lakini hii inamaanisha nini? Je, unapiganaje na dhambi kwa imani?
Tuseme ninajaribiwa kutamani. Picha fulani ya ngono inaingia kwenye ubongo wangu na kuniomba niifuatilie. Jinsi jaribu hili linavyopata nguvu ni kwa kunishawishi kuamini kuwa nitafurahi zaidi nikafuata. Nguvu ya majaribu yote ni matarajio kwamba itanifanya kuwa na furaha zaidi. Hakuna mtu anayetenda dhambi kwa sababu ya wajibu wakati anachotaka hasa ni kufanya haki.
"Imani si kuamini tu kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, bali pia kwamba yeye ni bora zaidi kuliko dhambi."
Kwa hiyo, nifanye nini? Watu wengine wangesema, “Kumbuka amri ya Mungu ya kuwa watakatifu ( 1 Petro 1:16 ) na utumie mapenzi yako kutii kwa sababu yeye ni Mungu!” Lakini kitu muhimu kinakosekana kwenye ushauri huu: imani . Watu wengi hujitahidi kuboresha maadili ambao hawawezi kusema, "Maisha ninayoishi sasa katika mwili ninaishi kwa imani " ( Wagalatia 2:20 ). Watu wengi hujaribu kupenda ambao hawatambui kwamba cha muhimu ni “ imani itendayo kazi kwa upendo” (Wagalatia 5:6). Vita dhidi ya tamaa (au uchoyo au woga au jaribu lingine lolote) ni pambano la imani. Vinginevyo, matokeo yake ni uhalali (kufuata sheria ili kupata wokovu).
Kupigana na Dhambi kwa Roho
Jaribio la kutamani linapokuja, Warumi 8:13 inasema: Mkiliua kwa Roho mtaishi. Kwa Roho! Hiyo ina maana gani? Kati ya silaha zote ambazo Mungu anatupa ili kupigana na Shetani, ni kipande kimoja tu kinachotumiwa kuua: upanga. Unaitwa upanga wa Roho ( Waefeso 6:17 ). Kwa hiyo, Paulo anaposema, “Ueni dhambi kwa Roho ,” ninachukua hiyo kumaanisha, “Mtegemee Roho, hasa upanga wake.”
Upanga wa Roho ni nini? Ni neno la Mungu ( Waefeso 6:17 ). Hapa ndipo imani inapoingia. “Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.” ( Warumi 10:17 ). Neno la Mungu linakata ukungu wa uongo wa Shetani na kunionyesha mahali ambapo furaha ya kweli na ya kudumu inapatikana. Na hivyo neno hunisaidia kuacha kutumainia uwezo wa dhambi kunifanya niwe na furaha, na badala yake hunishawishi kuiamini ahadi ya Mungu ya furaha (Zaburi 16:11).
Nashangaa ni waumini wangapi leo wanatambua kwamba imani si tu kuamini kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Imani pia ni kuwa na uhakika kwamba njia yake ni bora kuliko dhambi. Mapenzi yake ni ya busara zaidi. Msaada wake ni wa uhakika zaidi. Ahadi zake ni za thamani zaidi. Na malipo yake ni ya kuridhisha zaidi. Imani huanza na kutazama nyuma kwenye msalaba, lakini inaishi kwa kutazama mbele kwenye ahadi za Mungu. Abrahamu “bali alitiwa nguvu katika imani yake. . . akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi ” (Warumi 4:20–21). “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo” ( Waebrania 11:1 ).
Imani inapotawala moyoni mwangu, ninaridhika na Kristo na ahadi zake. Hiki ndicho Yesu alichomaanisha aliposema, “Yeye aniaminiye hataona kiu kamwe” ( Yohana 6:35 ). Ikiwa kiu yangu ya furaha na maana na shauku inatoshelezwa na uwepo na ahadi za Kristo, nguvu ya dhambi inavunjwa. Hatukubaliani na ofa ya nyama ya sandwich wakati tunaweza kuona nyama nzuri (steki) ikiiva kwenye grill.
Kuridhika Hupunguza Dhambi
"Ikiwa kiu yangu ya furaha na maana na shauku inatoshelezwa na Yesu, nguvu ya dhambi itakatika."
Vita vya imani ni vita vya kubaki kuridhika katika Mungu. “Kwa imani Musa . . . [aliacha] anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu . . . . [Alitazamia] thawabu ” (Waebrania 11:24–26). Imani haitosheki na “anasa za haraka.” Ina njaa kubwa kwa ajili ya furaha. Na neno la Mungu linasema, “Utanijaza na furaha mbele zako,pamoja na furaha za milele katika mkono wako wa kuume.” ( Zaburi 16:11 ). Kwa hiyo, imani haitakengeushwa na kuingia katika dhambi. Haitakata tamaa kirahisi hivyo katika utafutaji wake wa furaha kuu na kamili.
Jukumu la neno la Mungu ni kuilisha hamu ya imani kwa ajili ya Mungu. Na kwa kufanya hivi, kunaondoa moyo wangu mbali na ladha danganyifu ya tamaa. Mwanzoni, tamaa inaanza kunihadaa kuhisi kwamba ningekosa kuridhika sana ikiwa ningefuata njia ya usafi. Lakini basi ninachukua upanga wa Roho na kuanza kupigana.
Nilisoma kwamba ni afadhali kuling'oa jicho langu kuliko kutamani (Mathayo 5:29). Nilisoma kwamba nikifikiri juu ya mambo yaliyo safi na ya kupendeza na yaliyo bora, amani ya Mungu itakuwa pamoja nami (Wafilipi 4:7–8). Nilisoma kwamba kuweka nia katika mwili huleta kifo, lakini kuweka nia katika Roho huleta uzima na amani (Warumi 8: 6). Na ninapoomba ili imani yangu iridhishwe na maisha na amani ya Mungu, upanga wa Roho huitoa sukari inayofunika sumu ya tamaa. Ninaiona kama ilivyo. Na kwa neema ya Mungu, nguvu zake za kuvutia zimevunjwa.
Imani Inayo Kutazama Mbele
Hivi ndivyo wafu wanavyopigana na dhambi. Hii ndiyo maana ya kuwa Mkristo. Tumekufa kwa maana ya kwamba utu wa zamani wa kutokuamini (mwili) umekufa. Badala yake kuna uumbaji mpya. Kinachoifanya kuwa mpya ni imani. Siyo tu imani inayotazama nyuma katika kifo cha Yesu, bali imani inayotazamia mbele katika ahadi za Yesu. Sio tu kuwa na uhakika wa kile alichofanya, bali pia kuridhika na kile atakachofanya.
Huku umilele wote ukining'inia katika mizani, tunapigana vita vya imani. Adui yetu mkuu ni uongo unaosema kwamba dhambi itafanya maisha yetu yajayo kuwa ya furaha zaidi. Silaha yetu kuu ni kweli inayosema Mungu atafanya wakati wetu ujao uwe na furaha zaidi. Na imani ni ushindi ushindao uongo, kwa sababu imani imeridhika na Mungu.
“Changamoto Si kuifuata haki tu bali kuipendelea haki, kuyatafakari Maandiko kwa sala ili kupata furaha na amani katika kuziamini ahadi za Mungu”
Kwa hiyo, changamoto iliyo mbele yetu si tu kuyafanya yale ambayo Mungu anasema kwa sababu yeye ni Mungu, bali kuyatamani yale ambayo Mungu anasema kwa sababu yeye ni mwema. Changamoto si kuifuata haki tu, bali kuipendelea haki. Changamoto ni kuamka asubuhi na kuyatafakari Maandiko kwa sala hadi tupate furaha na amani katika kuamini “ahadi za thamani na kuu sana” za Mungu (Warumi 15:13 ; 2 Petro 1:4). Kwa furaha hii iliyowekwa mbele yetu, amri za Mungu hazitakuwa mzigo (1 Yohana 5: 3), na malipo ya dhambi yataonekana kuwa mafupi sana na hayawezi kutuvutia.
Commentaires