Makala imeandikwa na John Piper
Mwanzilishi na Mwalimu, desiringGod.org
Ikiwa hauna mpango mzuri wa jinsi utakavyokufa, labda mtu atawasha luninga tu.
Kama mhudumu wa neno la Mungu, daima nimefikiri kwamba sehemu ya wito wangu ni kuwasaidia watu kufa vizuri. Hilo linajumuisha lengo la Paulo kwamba Kristo atukuzwe katika mwili wake kwa kifo (Wafilipi 1:20). Nilifikiria mahubiri ya kila Jumapili kama sehemu ya maandalizi haya ya kifo. Na nilitumaini kwamba kila ziara pembeni ya kitanda cha wanaokufa itakuwa ya kuimarisha imani, kutoa tumaini, iliyojaa Biblia, inayozingatia injili, na kumwinua Kristo.
Ndio maana niliguna kwa huzuni pale hospitali nilipoona luninga iking'aa kwenye giza linalokaribia na kifo. Nilihisi haviendani kabisa. Ni ajabu.
Mmoja kati ya wanawake wacha-Mungu mno niliyowahi kumjua alikuwa anakufa. Alikuwa amejawa na Roho na maombi. Katika mojawapo ya ziara zangu hospitalini katika siku zake za mwisho, alinisihi nimuombee kifo chake kije haraka, na akaniambia kuhusu ndoto mbaya alizokuwa akipata za “wanawake waliovaa nusu uchi wakicheza na kuzunguka kitanda changu.” Nilijiuliza ikiwa kulikuwa na uhusiano na luninga ambayo wafanyakazi waliwasha.
Wengi wetu, tunapokaribia kufa, tutakuwa hafifu kifikra na kimwili hivyo hatutaweza kuandaa mipango. jipange sasa hivi.
Labda sivyo. Lakini kwa hakika sote tunaweza kukubaliana, kuna njia bora zaidi ya kuzitayarisha nafsi zetu "kukabiliana na Mwamuzi na Muumba wetu bila uwoga". Sehemu ya mpango wa kufa vizuri ni kuwa na marafiki wanaoshiriki maono yako ya jinsi ya kuishi na kufa kwa ajili ya utukufu wa Kristo. Wengi wetu, tunapokaribia kufa, tutakuwa hafifu kifikra na kimwili hivyo hatutaweza kuandaa mipango. Ni bora kuifanya hivi sasa.
Iwe mzee au kijana, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, fanya ifahamike kwamba unataka - na unahitaji - kifo kilichojaa Biblia, na kinachozingatia injili. Ninafikiria aina ya kifo ambacho John Knox alichagua.
"Nanga ya Kwanza" ya Knox
Ilikuwa Novemba 24, 1572. Knox alikuwa na umri wa miaka 57 au 58. (Mwaka wa kuzaliwa kwake haujulikani.) Nimonia ya kikoromeo ilikua inamuua. Wasifu mpya wa Jane Dawson unaelezea siku zake za mwisho.
Mke wake Margaret alikuwa karibu sana, isipokuwa alipokuwa akiwajali watoto wao watatu wa kike na wawili wa kiume. Richard Bannatyne, katibu mwaminifu na rafiki wa Knox, hakuondoka pembeni ya kitanda.
Majira ya saa kumi na moja jioni, alimuita mkewe. Hapo awali alikuwa ameomba kusomewa Isaya 53 na maneno matamu ya injili:
Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu, alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu; adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake, na kwa majeraha yake sisi tumepona.Sisi sote, kama kondoo, tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe, naye Bwana aliweka juu yake maovu yetu sisi sote. (Isaya 53:5-6).
Pia aliomba 1 Wakorintho 15 isomwe pamoja na maelezo yake ya kina kuhusu uhusiano kati ya ufufuo wa Kristo na ufufuo wake mwenyewe.
Lakini hatimaye, alimwomba mke wake asome “nanga yake ya kwanza” pendwa: Yohana 17. Miaka thelathini iliyopita, wakati Knox alipokuwa anakuja kwenye imani ya Marekebisho kutoka kwenye Ukatoliki wa Kirumi, hii ndiyo sura iliyomletea amani. Alisema, hapa ndipo “nilipotupa nanga yangu ya kwanza.” Hapa aliona mizizi ya uchaguzi na kujitolea kwa Kristo kuwatunza wale ambao Baba alimpa.
“Jina lako nimelidhihirisha kwa watu wale ulionipa kutoka katika ulimwengu. Walikuwa wako, ukanipa mimi, nao wamelishika neno lako. . . . Ninawaombea. Siuombei ulimwengu, bali wale ulionipa, kwa maana ni wako. . . . Baba Mtakatifu, uwalinde kwa jina lako ulilonipa. . . . Siombi uwatoe katika ulimwengu, bali uwalinde na yule mwovu. . . . Uwatakase katika ile kweli; neno lako ndiyo kweli.” ( Yohana 17:6 , 9 , 11 , 15 , 17 ). Margaret akaisoma sura yake ya nanga. Knox alisema, "Je, hiyo si sura ya kustarehesha?" Kifo kilimjia kama masaa sita baadaye.
Wakifikiri bado amelala, familia na marafiki zake walifanya maombi yao ya kawaida ya jioni baada ya saa 4 usiku. Alipoulizwa na Dk. Preston kama alikuwa amesikia zaburi zilizoimbwa na sala, Knox alijibu, “Ninamwomba Mungu kwamba ninyi na watu wote mzisikie kama mimi nilivyozisika; nami namsifu Mungu kwa sauti hiyo ya mbinguni.” Yapata saa 5 usiku, Robert Campbell akiwa ameketi kwenye kiti karibu na kitanda, alimsikia Knox akihema kwa muda mrefu, akalia, na kusema, "Sasa imekamilika." Alipoombwa na Bannatyne atoe ishara kuonyesha kwamba alikumbuka ahadi za Kristo, Knox aliinua mkono wake kwa mara ya mwisho na “akalala bila maumivu yoyote.” Vita vya Knox vilikuwa vimeisha. (Knox, 310)
Ndiyo, na vita vilipigwa hadi mwisho kwa neno la Mungu. Kilikuwa ni kifo kilichojaa Biblia. Hiki ndicho alichoomba, na hiki ndicho alichopewa na mkewe na marafiki zake.
Tayari kwa ajili ya Mbingu
Kuimba na kunena neno la Mungu - hivi ndivyo ninavyotarajia kusikia ikiwa kifo changu kitakuja polepole. Ikiwa hujawahi kupenda kusoma neno la Mungu na kuimba ukweli wa injili, tafakari kwa kina maneno ya Knox, “Namsifu Mungu kwa sauti hiyo ya mbinguni.”
Hakuna kitakachokuwa na mfarakano katika saa hiyo ya mwisho kuliko luninga. Na hakuna kitu kitamu kuliko "sauti ya mbinguni" ya marafiki wanaoimba na kusoma neno la Mungu. Iliyojaa injili, iliyojaa Kristo, iliyojaa tumaini. Jipangie hili.
Comments