top of page

Usiibadhiri Saratani Yako



Makala imeandikwa na John Piper

Mwanzilishi na Mwalimu, desiringGod.org


Ninaandika haya usiku kabla ya operesheni yangu ya upasuaji wa tezi dume. Ninaamini katika uwezo wa Mungu wa kuponya - kwa miujiza na kwa dawa. Ninaamini ni sawa na vizuri kuombea aina zote mbili za uponyaji. Saratani haibadhiriwi ikiponywa na Mungu. Anapata utukufu, na ndiyo sababu ya uwepo wa saratani. Kwa hivyo, kutokuombea uponyaji kunaweza kubadhiri saratani yako. Lakini uponyaji sio mpango wa Mungu kwa ajili ya kila mtu. Na kuna njia zingine nyingi za kubadhiri saratani yako. Nina omba kwa ajili yangu na yako ili tusibadhiri maumivu haya.

Maana ya Kudabhiri

"Badhiri" inamaanisha kutumia kitu bila maana au kupoteza bila faida yoyote kwa uzembe.

1. Utaibadhiri saratani yako ikiwa huamini kwamba Mungu aliitengeneza kwa ajili yako.


Haitoshi kusema kwamba Mungu anaitumia saratani yetu tu, lakini haitengenezi. Kile ambacho Mungu huruhusu, huruhusu kwa sababu. Na sababu hiyo ni mpango wake. Ikiwa Mungu anaona maendeleo ya molekuli kuwa saratani, anaweza kuizuia au la. Asipofanya hivyo, ana kusudi. Kwa kuwa yeye ni mwenye hekima isiyo na kikomo, ni sawa kuita kusudi hili mpango. Shetani yupo kikweli na husababisha raha na maumivu mengi. Lakini yeye si mkuu. Kwa hiyo, anapompiga Ayubu na majipu (Ayubu 2:7), Ayubu anahusisha jambo hilo kwa Mungu (Ayubu 2:10) — na mwandikaji aliyevuviwa anakubali: “Wao . . . Walimfariji kwa ajili ya mabaya yote ambayo Bwana alileta juu yake” (Ayubu 42:11). Ikiwa huamini kwamba Mungu alikutengenezea saratani yako, utaipoteza.


2. Utaibadhiri saratani yako ukiamini ni laana na sio zawadi.


"Lengo la Mungu katika saratani yetu ni kuvigonga vile tunavyojitegemeza kutoka chini ya mioyo yetu ili tumtegemee yeye pekee."

“Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu” (Warumi 8:1). "Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu" (Wagalatia 3:13). “Hakuna uchawi dhidi ya Yakobo,wala hakuna uaguzi dhidi ya Israeli.” (Hesabu 23:23). “Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao, Bwana hutoa wema na heshima; Hakuna kitu chema anachowanyima wale ambao hawana hatia. (Zaburi 84:11).


3. Utaibadhiri saratani yako ikiwa unatafuta faraja kutoka kwenye uwezekano wako wa kupona badala ya kutoka kwa Mungu.


Mpango wa Mungu katika saratani yako sio kukufundisha hesabu ya kimantiki, ya uwezekano wa kibinadamu.  Ulimwengu unapata faraja kutokana na uwezekano wao wa kupona.  Si Wakristo. Wengine huhesabu magari yao (asilimia ya kunusurika) na wengine huhesabu farasi zao (madhara ya matibabu), "lakini sisi tunatumaini katika jina la Bwana, Mungu wetu" (Zaburi 20:7).


Mpango wa Mungu uko wazi katika andiko la 2 Wakorintho 1:9: “Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo. Ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu.” Kusudi la Mungu katika saratani yetu (miongoni mwa maelfu ya mambo mengine mazuri) ni kuvitoa vifaa tunavyotegema kutoka chini ya mioyo yetu ili tumtegemee yeye kabisa.


4. Utaibadhiri saratani yako ikiwa utakataa kufikiria juu ya kifo.


Sisi sote tutakufa, ikiwa Yesu ataahirisha kurudi kwake. Kutofikiria jinsi itakavyokuwa kuyaacha maisha haya na kukutana na Mungu ni upumbavu. Andiko la Mhubiri 7:2 linasema, “Afadhali kwenda kwenye nyumba ya msiba kuliko kwenda kwenye nyumba ya karamu; Unawezaje kuliweka moyoni ikiwa hutalifikiria? Zaburi 90:12 inasema, “Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri,ili tujipatie moyo wa hekima.” Kuhesabu siku zako kunamaanisha kufikiria jinsi zilivyo chache na kwamba zitaisha. Utapataje moyo wa hekima ukikataa kuwaza juu ya hili? Ni upotevu wa aina gani, ikiwa hatufikiri juu ya kifo.


5. Utaibadhiri saratani yako ikiwa unafikiri kwamba "kuishinda" saratani kunamaanisha kubaki hai badala ya kumthamini Kristo.


“Saratani haishindi ukifa. Itashinda ikiwa utashindwa kumthamini Kristo.”

Mipango ya Shetani na Mungu katika saratani haiko sawa. Shetani anakusudia kuharibu upendo wako kwa Kristo. Mungu anakusudia kuukuza upendo wako kwa Kristo. Saratani haishindi ukifa. Itashinda ikiwa utashindwa kumthamini Kristo. Mpango wa Mungu ni kukuondoa katika kifua cha ulimwengu na kukusherehekea kwenye utoshelevu wa Kristo. Imekusudiwa kukusaidia kusema na kuhisi, “Nahesabu kila kitu kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu Bwana wangu.” Na kwa hiyo kujua kwamba, “Kuishi ni Kristo, na kufa ni faida” (Wafilipi 3:8; 1:21).


6. Utaibadhiri saratani yako ikiwa unatumia muda mwingi kusoma habari za saratani na kukosa muda wa kutosha wa kusoma kuhusu Mungu.


Si vibaya kujua kuhusu saratani. Ujinga sio fadhila. Lakini mvuto wa kujua zaidi na zaidi na ukosefu wa bidii ya kumjua Mungu zaidi na zaidi ni dalili ya kutoamini. Saratani inakusudiwa kutuamsha kwa uhalisia wa Mungu. Imekusudiwa kuweka hisia na nguvu nyuma ya amri, “Tumkubali Bwana, tukaze kumkubali yeye.” (Hosea 6:3).  Imekusudiwa kutuamsha tuone ukweli wa Danieli 11:32: “Watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti.” Imekusudiwa kutufanya tuwe miti ya mialoni isiyotikisika, isiyoweza kuharibika: “Bali huifurahia sheria ya Bwana,naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana. Mtu huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, ambao huzaa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Lolote afanyalo hufanikiwa.” (Zaburi 1:2–3). Ni ubadhiri wa kiasi gani wa saratani ikiwa tunasoma usiku na mchana kuhusu saratani na sio juu ya Mungu.


7. Utaibadhiri saratani yako ikiwa utairuhusu ikupeleke kwenye upweke badala ya kuimarisha mahusiano yako na mapenzi dhahiri.


Epafrodito alipomletea Paulo zawadi zilizotumwa na kanisa la Filipi, aliugua karibu kufa. Paulo anawaambia Wafilipi, “Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa.” (Wafilipi 2:26). Ni jibu la kushangaza kama nini! Haisemi kwamba walihuzunika kwamba alikuwa mgonjwa, bali kwamba alihuzunika kwa sababu walisikia kwamba alikuwa mgonjwa. Hiyo ndiyo aina ya moyo ambao Mungu analenga kuuumba na saratani: moyo wa upendo wa dhati, unaowajali watu. Usibadhiri saratani yako kwa kujirudia nyuma ndani yako mwenyewe - yaani, kujificha na kujitenga na watu.


8. Utaibadhiri saratani yako ikiwa utahuzunika kama wale ambao hawana matumaini.


Paulo alitumia msemo huu kuhusiana na wale ambao wapendwa wao walikuwa wamekufa: “Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini.” (1 Wathesalonike 4:10; 13). Kuna huzuni wakati wa kifo. Hata kwa mwamini anayekufa, kuna hasara ya muda: kupoteza mwili, kupoteza wapendwa hapa duniani, kupoteza huduma ya kidunia. Lakini huzuni ni tofauti - imejawa tumaini. “Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana.” (2 Wakorintho 5:8). Usiibadhiri saratani yako kuomboleza kama wale ambao hawana tumaini hili.


9. Utaibadhiri saratani yako ikiwa utaiona dhambi kuwa ya kawaida kama hapo awali.


Je, dhambi zako zinazokusumbua zinavutia kama zilivyokuwa kabla ya kuugua saratani? Ikiwa ndivyo, unaibadhiri saratani yako. Saratani imeundwa kuharibu hamu ya dhambi. Kiburi, uchoyo, tamaa, chuki, kutosamehe, kutokuwa na subira, uvivu, kuahirisha mambo - hawa wote ni maadui ambao saratani inakusudiwa kuwashambulia. Usifikirie tu kupigana dhidi ya saratani. Fikiria pia kupambana pamoja na saratani. Mambo haya yote ni maadui wabaya kuliko saratani. Usiibadhiri nguvu ya saratani kuwaangamiza maadui hawa. Acha uwepo wa umilele ufanye dhambi za wakati zionekane kuwa bure kama zilivyo kweli. “Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake?” (Luka 9:25).


10. Utaibadhiri saratani yako ikiwa utashindwa kuitumia kama njia ya kushuhudia ukweli na utukufu wa Kristo.


Wakristo hawako popote kwa bahati mbaya ya kimungu. Kuna sababu za kwanini tunaishia pale tunapoishia. Fikiria yale ambayo Yesu alisema kuhusu hali zenye kuumiza na zisizopangwa: “Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kuwafunga magerezani. Nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu. Hii itawapa nafasi ya kushuhudia. ” ( Luka 21:12–13 ).


"Ikiwa huamini kwamba Mungu alikutengenezea saratani yako, utaibadhiri."

Ndivyo ilivyo na saratani. Hii itakuwa fursa ya kutoa ushahidi. Kristo anastahili milele. Hapa kuna fursa nzuri ya kuonyesha kwamba ana thamani zaidi ya maisha. Usiibadhiri.


Kumbuka, haujaachwa peke yako. Utapata msaada unaohitaji. “Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu” (Wafilipi 4:19).

 


Comments


bottom of page