top of page

Wakalvini Wanapaswa Kuwa Watulivu na Wema Zaidi Kuliko Wote



Makala imeandikwa na David Mathis

Mhariri Mtendaji, desiringGod.org


Vifafanuzi vichache ni vya kusikitisha zaidi kwa Mkalvini kuliko hasira na udhalimu.


Je, wale wanaounga mkono Ukuu wa Mungu wangewezaje kuchukua sehemu ya washitushaji katika siku ya kuharibika kwa jamii? Na watu wanaopenda “mafundisho ya neema” bila kujificha wangewezaje kuwatendea wengine bila fadhili? Sisi Wakalvini tunaamini ushuhuda wa wazi wa Biblia kwamba Mungu ni mkuu katika wokovu na ni mkuu juu ya kila kitu. Je, tumeshindwaje kuona kwamba kuwachokonoa wengine machoni—macho tunayoamini kwamba Mungu bado hajayafungua—ni sawa na kumdhihaki Mungu mwenyewe?


“Wakalvini wanapaswa kuwa wapole na wenye subira zaidi kuliko watu wote,” aliona mchungaji mpendwa na mwandishi wa nyimbo John Newton (1725–1807). Ikiwa tunaamini kweli kile tunachosema, sisi Wakalvini tunapaswa kuwa watu watulivu na wema zaidi, bila kujali jinsi ulimwengu wetu unavyokuwa na hasira na udhalimu. Na tunapaswa kuwawajibisha wenzetu wanaomuungama Mungu mkuu wanapoonyesha hasira kwa kutokuamini au ukatili kwa wale ambao hawashiriki theolojia yetu ya neema nyingi.


Hata hivyo, sisi pia hatupaswi kushtuka wakati Wakalvini wakishindwa kuishi kulingana na neema wanayodai. Baada ya yote, tunaamini katika upotovu kamili pia. Sio udhuru, lakini pia hatupaswi kushangaa.


“Sisi wanadamu tuna uwezo wa kupotosha karibia fundisho lolote la kweli na kuligeuza kuwa kitu kibaya,” asema mwandishi na profesa DA Carson, mwanzilishi wa The Gospel Coalition . "Inawezekana kwa kutumia moyo usiyofaa kuyachukua mafundisho haya na kuanza kujiona sisi kama dhehebu bora zaidi. Inaweza kuzaa aina fulani ya kiburi.”


Je, Wakalvini Wamejitayarisha Vyema kwa ajili ya Maumivu?

Uhalisia mmoja wa kusikitisha ni Mkalvini mwenye hasira . Tabia tete zitatokea katika enzi yoyote, lakini tunaweza kukabiliwa nayo hasa katika siku zetu za kuzorota kwa jamii. Na swali ni kubwa zaidi kadiri upinzani unavyoongezeka kuelekea Ukristo wa kibiblia.


Kuamini kwamba Mungu ni mwema kabisa na anatawala kabisa kunapaswa kutufanya tuwe wapole na wavumilivu zaidi, lakini je,haipaswi pia kutufanya tuwe watulivu zaidi katikati ya misukosuko ya kitamaduni? Nilimuuliza Carson ikiwa kuibuka upya kwa Wakalvini wa kizazi kilichopita kunapaswa kutufanya tuwe tayari zaidi kukabiliana na shinikizo linalokuja, na hata mateso dhidi ya Wakristo.

“Ningependa kufikiria hivyo. Ningesema hakika inapaswa kutufanya hivyo. Hasa kuamini kabisa katika majaliwa ya Mungu katika mambo kama hayo ili usifikirie, 'Loh! Mungu anampoteza huyu,' au kitu kama hicho. Ndiyo, inapaswa."


Lakini bila shaka, tuna mengi ya kusema kuliko tu kile kinachopaswa kuwa. Tunazijua dhambi zetu.

"Sitaki kusema kwamba kwa sababu wewe ni Mkalvini, basi una kinga zaidi dhidi ya mikazo ya enzi," aongeza Carson. "Afadhali niseme, 'Ikiwa unajiita Mkalvini, jifunze kuamini wema mkuu wa Mungu.' Huu si wakati wa kujiona washindi au kujiona tuko bora zaidi. Huu ni wakati wa kutubu na kumwomba Mungu rehema.”


Ukuu Wa Mungu Unajaza Ombwe

Sababu ya kuzuka upya kwa theolojia ya ukubwa wa Mungu katika siku zetu, kulingana na Carson, ni ile “theolojia ya kiinjili ya kiwango cha chini kabisa iliyokubaliwa na kizazi kilichopita na itikio dhidi yake. . . . Ilikuwa rahisi sana kusema - 'Mwamini Yesu na umpokee kama Mwokozi wako binafsi na kila kitu kitaenda vizuri.' Watu walikuwa wakitafuta uhalisi zaidi, kitu chenye nguvu zaidi, kitu kilichokuwa na nguvu ya kubadilisha - si kile kilichokuja kuwa aina ya imani rahisi.


Theolojia ya Biblia ya Mungu-mkubwa isiyo fifishwa imejaza pengo na kuwaandaa wengi kuwa tayari kwa ajili ya matusi, kashfa, na upinzani utakaowalenga Wakristo waaminifu katika enzi hii inayozidi kuongozwa na wasomi wa kilimwengu. Theolojia ya neema ya bure ya Mungu - licha ya dhambi zetu, katika kuchaguliwa, katika upatanisho, katika uongofu, katika uvumilivu, na katika mambo yote - inaweza na inapaswa kutufanya kuwa watu watulivu zaidi, hata wakati ulimwengu unaotuzunguka unaonekana kutetemeka.


Hakuna Cha Kuvutia Kuhusu Mateso

Kwa majaliwa ya Mungu, ufufuo wa Wakalvini unaweza kuwa ulikuja kwa wakati ufaao ili kuwapa Wakristo wengi nguvu zinazohitajika kwa ajili ya dhoruba zinazokuja. Hata hivyo, na isemwe kwa sauti kubwa na wazi kwamba kuamini mamlaka kuu ya Mungu hakutupelekei tuyaone manyanyaso kuwa yenye mvuto.  Carson anajua vyema zaidi kutokana na mapito yake binafsi, alikua Mbaptisti aliyeteswa katika Kanada ya kifaransa katikati ya karne ya ishirini iliyochukia Waprotestanti.


“Nakumbuka nilipokulia, kulikuwa na fundi viatu. Siku hizo, huyu si mtu ambaye anauza viatu kwenye duka la viatu. Alitengeneza viatu kweli. Aliipima miguu ya watu na kuwatengenezea viatu. Aliishi katika kijiji kidogo cha Saint Cyril. Alijulikana. Alikuwa mfanyabiashara mdogo akifanya kazi zake. Alipoongoka, vyema na kwa uwazi kabisa, na akapoteza 90% ya biashara yake. Hakujua jinsi gani angeweza kufanikiwa. Kisha biashara yake ikachomwa moto. Yeye na familia yake walihama kutoka jimbo la Quebec na kuhamia Ontario.


"Kweli, ilikuwa ni kuhama kwa lazima kwake. Ilibidi aanze kujifunza Kiingereza. Hakujua Kiingereza kingi kabla ya hapo. Lakini pia, kwenye mtazamo wa kanisa letu, ilikuwa ni hasara kubwa sana. Alikuwa mwongofu wa kweli ambaye, kwa mtazamo wetu, alishindwa na mateso huko Kanada ya kifaransa. Kulikuwa na mambo mengi kama hayo. Huu ni mfano uliokithiri.  Lakini ilitokea.


"Ikiwa unajiita Mkalvini, basi jifunze kuuamini wema mkuu wa Mungu."

“Shinikizo unalokabiliana nalo kutokana na mambo ya aina hiyo halikujazi furaha unapoyapitia. Kwa kutazama nyuma, unaweza kuona katika picha kubwa jinsi Mungu alivyotumia hilo kuwakomaza watu na kuwatayarisha kwa kipindi cha kuzaa matunda ambacho kilikuja miongo miwili au mitatu baadaye. Lakini wakati unaipitia hiyo miongo miwili au mitatu, hakuna kitu cha kuvutia kuhusu mapito hayo.”


Je, Theolojia Yako Imekunyenyekeza?

Ukweli wa pili wa kusikitisha ni Mkalvini asiye na huruma. Yafaa tujiulize mara kwa mara, je, tunaakisi theolojia tunayokiri kwa usahihi kwa jinsi tunavyowatendea wengine? Iwe inaonekana kuwa kubwa kama shinikizo la kijamii na msukosuko wa kijamii, au inaonekana kuwa ndogo kama mazungumzo ya kila siku na wasioamini na aina zingine za Wakristo, sisi tunaodai ukuu wa Mungu tuna uhuru wa kuwa watulivu kuhusu ulimwengu, lakini pia kuwa mwema kwa watu wake.


Newton, haswa, alikuwa na maneno ya upole, lakini yenye kujenga kwa Wakalvini ambao walikuwa wagumu kwa wengine ambao hawakushiriki theolojia yao. Aliwakumbusha, “Theolojia yenye kunyenyekesha ya Ukalvini inadhoofishwa na maneno yenye uchungu, hasira, na dharau,” naye akauliza kwa uwazi, “Je, Ukalvini wenu umewanyenyekeza?” Kama vile Tony Reinke anavyonukuu kutoka kwa maisha ya Newton, "Ukalvini, ukieleweka vyema, hutunyenyekesha, na hilo linapaswa kuwa wazi kwa wengine."


“Theolojia yenye kunyenyekesha ya Ukalvini inadhoofishwa na maneno yenye uchungu, hasira, na dharau.”

Newton alikuwa na shida kidogo ya kumpata "Mkalvini mwenye kiburi na anayejitosheleza" katika siku zake na akaonya, "Ninaogopa kwamba kuna wakalvini, ambao, ingawa wanahesabu kuwa ni uthibitisho wa unyenyekevu wao kwamba wako tayari kwa maneno kumdhalilisha kiumbe na kumpa Bwana utukufu wote wa wokovu, walakini hawajui ni roho ya namna gani waliyo nayo.”


Ushauri wa Newton ni wa busara - na wa kuhukumu. Unapotofautiana na “mtu ambaye hajaongoka,” kumbuka kwamba “yeye anafaa zaidi kupokea huruma yako kuliko hasira yako.” Na ikiwa yeye ni mwamini mwenzetu katika Yesu?


Bado kitambo kidogo mtakutana mbinguni; basi atakuwa karibu zaidi kwako kuliko rafiki wa karibu zaidi uliye naye duniani sasa. Tazamia kipindi hicho katika mawazo yako; na ijapokuwa unaweza kuona ni muhimu kuyapinga makosa yake, muone yeye binafsi kama nafsi ya ndugu, ambaye unapaswa kuwa na furaha pamoja naye katika Kristo milele.


Kama vile ushauri kama huo ulivyokuwa katika siku za Newton, labda ni wa kinabii zaidi katika siku zetu, ambapo mistari imechorwa kidogo kati ya madhehebu, na zaidi kati ya imani na kutoamini.


Kwa sababu Mungu ni Mwema

Hata hivyo, mwishowe, sio makisio tu ya kitheolojia ambayo yatatufanya kuwa wapole. Wakristo hawawi wapole - si kwa wema unaotokana na Roho - kwa kutafakari tu miunganisho isiyoeleweka, bali kwa kuzilisha roho zetu, na kuchukua vidokezo vyetu kutoka kwenye maneno yenyewe ya Mungu.


Sio tu kwamba hadithi ya kanisa la kwanza husherehekea matendo madogo ya fadhili (Matendo 10:33 ; 24:4 ; 27:3 ; 28:2), lakini pia kifungu baada ya kifungu kinabainisha mwenendo wa Kikristo kuwa wa fadhili dhahiri (2 Wakorintho 6:6 ; Wakolosai 3:12 ; Tito 2:5). Sio tu kwamba viongozi wanaotambuliwa kanisani wanapaswa kuwa "wema kwa kila mtu" (2 Timotheo 2:24), lakini pia Wakristo wote wanapaswa kuwa "wema kwa kila mmoja" (Waefeso 4:32). Wema ni tunda la Roho (Wagalatia 5:22). Upendo huvumilia na hufadhili (1 Wakorintho 13:4).


“Fadhili za Mungu mwenyewe hutuweka huru kuelekeza wema wetu katika maisha ya wengine.”

Na Mungu, ambaye anatawala juu ya kila inchi ya mraba ya ulimwengu, anapotuagiza kusitawisha fadhili, anatuchochea tukue kama waigaji wake wakubwa zaidi. Baba yetu wa mbinguni, asema Yesu, “ni mwema kwa wasio na shukrani na waovu” (Luka 6:35). Kwa wema wake, “yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” (Mathayo 5:45). Fadhili kama hizo "zinakusudiwa kukuongoza kwenye toba" (Warumi 2:4). Wema kama huo huwaingiza hata wageni katika mti wake wa baraka wa zamani kwa imani (Warumi 11:22).


Kwa sababu tumeokolewa kupitia “wema na upendo” wa Mungu (Tito 3:4), na kutazamia umilele tukiwa na “wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu.” (Waefeso 2:7), tunawekwa huru kuzielekeza fadhili zake kwetu kuelekea kwenye maisha ya wengine.


Ukalvini unapaswa kututayarisha vyema kuteseka na upinzani - na sio kuwaonea wengine. Tunasema tunaamini ni Mungu pekee ndiye anayeweza kubadilisha mioyo, na hii inapaswa kutuachilia kuwa watu watulivu na wema kuliko wote.


Kama Carson anavyosema, "Ikiwa unajiita Mkalvini, basi jifunze kuamini wema mkuu wa Mungu."

Comments


bottom of page