Makala imeandikwa na John Piper
Mwanzilishi na Mwalimu, desiringGod.org
Wakati tishio la kifo linapogeuka kuwa mlango wa kuingia peponi, Wakristo wanakua huru kupenda hata iweje.
Kwa kuiondoa hatari ya milele, Kristo anawaita watu wake kwenye hatari ya kudumu ya muda mfupi.
Kwa wafuasi wa Yesu hatari ya mwisho imetoweka. "Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu" (Warumi 8:1). "Sio umauti, wala uzima... zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu" (Warumi 8:38-39). "Baadhi yenu watawaua .... Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia..” (Luka 21:16 , 18) "Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi" (Yohana 11:25).
Wakati tishio la kifo linapogeuka kuwa mlango wa kuingia peponi, kizuizi cha mwisho cha hatari ya muda kinavunjwa. Mkristo anaposema kutoka moyoni, “Kuishi ni Kristo na kufa ni faida,” yuko huru kupenda hata iweje. Aina fulani za Uislamu wenye itikadi kali zinaweza kuwashawishi wauaji ambao hujitoa muhanga kwa ndoto zinazofanana, lakini tumaini la Kikristo ni nguvu ya kupenda, si kuua. Tumaini la Kikristo huzalisha watoa maisha, si wachukua maisha. Kristo aliyesulubiwa anawaita watu wake kuishi na kufa kwa ajili ya adui zao, kama yeye alivyofanya. Hatari pekee zinazoruhusiwa na Kristo ni hatari za upendo. "Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia, Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya" (Luka 6:27-28).
Kwa kutoa ahadi zenye kushangaza za furaha ya milele, Yesu alianzisha harakati za watu wenye upendo wanaohatarisha maisha yao. “Mtasalitiwa hata na wazazi . . .na baadhi yenu watawaua” (Luka 21:16). Baadhi tu. Ambayo inamaanisha kwamba inaweza kuwa wewe na inaweza kuwa mwingine. Hiyo ndiyo maana ya kujihatarisha. Hamna hatari katika kujipiga risasi kichwani. Matokeo yake ni ya uhakika. Ni hatari kumtumikia Kristo katika eneo la vita. Unaweza kupigwa risasi. Au huenda usipigwe.
Kristo anatuita tujihatarishe kwa makusudi ya ufalme. Karibia kila ujumbe unaohimiza ununuzi wa kimarekani unasema kinyume: Ongeza faraja na usalama wako - hapa duniani, sio mbinguni. Kristo hasemi sawa nao. Kwa kila mtakatifu mwenye woga, anayeyumba-yumba kwenye ukingo wa mradi fulani hatari wa injili, Yesu anasema, “Usiogope, wanaweza kukuua tu” (Luka 12:4). Ndiyo, iongeze furaha yako kwa bidii zote! Kivipi? Kwa ajili ya upendo, hatari ya kutukanwa na kuteswa na kusemewa uongo, “kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni” (Mathayo 5:11-12).
Kuna urithi mkubwa wa kibiblia wa watu wenye upendo waliohatarisha maisha yao. Yoabu akiwakabili Washami upande huu na Waamoni upande huu, akamwambia Abishai ndugu yake, “Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Bwana atafanya lile lililo jema machoni pake" (2 Samueli 10:12). Esta alivunja sheria ya kifalme ili kuokoa watu wake na kusema, “Ikiwa ni kuangamia na niangamie.” (Esta 4:16). Shadraka na wenzake walikataa kuinamia sanamu ya mfalme na kusema, “Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa... Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”— Danieli 3:16-18 . Na Roho Mtakatifu alipomwambia Paulo kwamba katika kila mji vifungo na mateso vinamngoja, alisema, “Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano” (Matendo 20:24).
"Kila Mkristo alijua kwamba hivi punde au baadaye angelazimika kushuhudia imani yake kwa gharama ya maisha yake"
“Kila Mkristo,” alisema Stephen Neil kuhusu kanisa la kwanza, “alijua kwamba hivi punde au baadaye angelazimika kushuhudia imani yake kwa gharama ya maisha yake” (A History of Christian Missions, Penguin, 1964, uk. 43). Hii ilikuwa kawaida. Kuwa Mkristo ilikuwa ni kuhatarisha maisha yako. Makumi ya maelfu walifanya hivyo. Kwa nini? Kwa sababu kufanya hivyo ilikuwa ni kumpata Kristo, na kutofanya hivyo ni kupoteza nafsi yako. "Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata." (Mathayo 16:25).
Ndani ya Amerika na duniani kote gharama ya kuwa Mkristo halisi inapanda. Mambo yanarudi katika hali ya kawaida katika "zama hii mbaya ya sasa." Kwa kuongezea 2 Timotheo 3:12 italeta maana: "Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa." Wale waliofanya kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya injili kuwa mtindo wao wa maisha kwa hiari watakuwa tayari zaidi wakati hatuna chaguo. Kwa hiyo nawasihi, kwa maneno ya kanisa la kwanza, “Kwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba. Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.” ( Waebrania 13:13-14 ).
Mungu alipoziondoa hatari zote hapo juu
Alizifungulia hatari elfu za upendo.
- Mchungaji John
Comentarios